Published 2024-05-16 10:40:26 by JKCI
Zaidi ya asilimia 60 ya watu wenye shinikizo la juu la damu hapa nchini hawajitambui kama wana tatizo hilo kwani tafiti zinaonesha kati ya watu kumi watu watatu ndio wanatambua kuwa na tatizo hilo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Hospitali ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dar Group Dkt. Tulizo Shemu leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu siku ya shinikizo la damu duniani inayoadhimishwa kila ifikapo Mei 17.
Dkt. Shemu alisema Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu unatokana na madhara ya kiwango cha presha kuwa kikubwa katika mwili wa binadamu hivyo kusababisha shinikizo la damu kuwa juu.
“Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu hauna dalili maalumu lakini zipo dalili chache zinazoweza kujitokeza endapo mtu atapata ugonjwa huu zikiwemo dalili ya kuumwa kichwa mara kwa mara, macho kutoona vizuri, moyo kwenda haraka, pamoja na kubanwa na kifua”, alisema Dkt. Shemu
Dkt. Shemu alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inaenda kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya upimaji bila gharama tarehe 16 na 17 May 2024 katika Hospitali ya JKCI Dar Group lengo likiwa kuleta uelewa na ufahamu katika jamii kuhusu tatizo la shinikizo la juu la damu.
“Kauli mbiu ya mwaka huu inatutaka kuzifahamu tarakimu za shinikizo la damu kwa kupima presha kwa usahihi na endapo utakutwa na ugonjwa huu hakikisha unapata matibabu na kudhibiti ugonjwa ili usiweze kukuletea madhara mengine yatokanayo na tatizo la presha”, alisema Dkt. Shemu
Dkt. Shemu alisema kwa takwimu zilizofanyika kwa wagonjwa wanaotibiwa JKCI mwaka 2023 kati ya wagonjwa 125,927 waliopatiwa matibabu asilimia 42 walikuwa na shinikizo la juu la damu.
“Madhara ya ugojwa huu ni pamoja na kupata kiharusi, kusababisha figo kushindwa kufanya kazi, kupata magonjwa ya mshtuko wa moyo, tatizo la moyo kushindwa kufanya kazi, kuvimba miguu, kupata ganzi sehemu za mwili, kupumua kwa shida, kukosa nguvu pamoja na shida za uzazi”, alisema Dkt. Shemu
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sulende Kubhoja alisema tatizo la shinikizo la juu la damu huwapata pia watoto na tatizo hilo hutokana na matatizo mengine ambayo mtoto anakuwa nayo.
Dkt. Kubhoja alisema tunapoenda kuadhimisha siku ya shinikizo la damu tusiwasahau watoto kuwashirikisha upande wa kufanyiwa uchunguzi na hata eneo la kupata elimu kuhusu ugonjwa huo ili pale wanapoweza kujikinga wajikinge.
“Mara nyingi ukimkuta mtoto ana shinikizo la juu au la chini la damu hutokea kama mtoto ana matatizo ya figo, au matatizo mengine katika viungo vinavyowasiliana mwilini”, alisema Dkt. Kubhoja
Dkt. Kubhoja alisema kuna watoto wamekuwa wakipata tatizo la shinikizo la juu la damu kutokana na magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa pamoja na matatizo ya mishipa ya damu kuwa na hitilafu.
“Sisi tunapopata mtoto ana tatizo la shinikizo la juu la damu tunamfanyia uchunguzi kwa kuangalia kila kiungo cha mwili wa mtoto ili tuweze kutambau sehemu yenye matatizo na kuweza kuitibu” alisema Dkt. Kubhoja